Bilioni 60 zatengwa kwa ajili ya mikopo isiyo na riba kwa wajasiriamali Zanzibar

By: | Blog | April 23, 2024 10:32

Zanzibar 12 Februari 2022 – Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amepongeza jitihada za Benki ya CRDB katika kusaidiana na Serikali kuwawezesha wajasiriamali visiwani humo. Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo katika uzinduzi wa Mikopo isiyo na riba kwa Wajasiriamali iliyopewa jina la “INUKA NA UCHUMI WA BULUU” ikiwa ni ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya CRDB, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idris Abdulwakil, Kikwajuni Zanzibar. Katika hotuba yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa mikopo hiyo itakuwa kichocheo kikubwa kwa ukuaji wa uchumi wa Zanzibar. Amewataka wajasiriamali katika visiwa vya Unguja na Pemba kuchangamkia fursa hiyo ya kipekee kukuza mitaji na kuboresha biashara zao. Alisema kuwa juhudi zinazofanywa na Benki ya CRDB katika kujenga uchumi wa Zanzibar ni nyingi na anaamini kwamba sasa zinafahamika vizuri na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika na kudumisha uhusiano mwema uliopo kwa faida ya pande zote mbili pamoja na wateja wote kwa jumla. “Benki ya CRDB leo mmedhihirsha uzalendo wa kweli kwa kuandika historia ya kuwa Benki ya kwanza nchini kutoa mikopo bila riba kwa wajasiriamali. Hii inaonyesha dhamira ya kweli mliyonayo katika kuboresha maisha ya wajasiriamali hapa Zanzibar,” amesema Rais Mwinyi. Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa imani yake ni kwamba wajasiriamali wote watatoa ushirikiano mzuri kwa Benki ya CRDB na watachangamkia ipasavyo fursa zilizopo kwa kuzingatia taratibu zinazoongoza na kusimamia mikopo hiyo. Aliongeza kuwa vile vile wana uwezo na taaluma ya ujasiriamali, waadilifu na wana dhamira ya dhati ya kurejesha fedha hizo. Alieleza kwamba mikakati ya Serikali ya kuwawezesha Wajasiriamali aliyoahidi sasa inatimia ikiwa ni pamoja na utoaji wa vitambulisho, ujenzi wa masoko, utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu, elimu, zana, mitaji, maeneo bora ya kufanyia kazi pamoja na utaratibu mzuri wa ulipaji kodi. Aliwaahidi wajasiriamali kwamba Serikali itaendelea na juhudi za kuwapatia mitaji, masoko, elimu pamoja na kuweka mazingira rafiki ili waweze kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.

Rais Mwinyi alitoa pongezi hizo wakati wa uzinduzi wa program ya “INUKA NA UCHUMI WA BULUU” ambayo inalenga kuwawezesha wajasiriamali kupitia mikopo isiyo na riba, pamoja na mafunzo ya namna bora ya uendeshaji biashara.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema Benki hiyo inalichukulia kundi la wajasiriamali kama kundi la kimkakati katika maendeleo ya Taifa kutokana na kujumuisha asilimia kubwa ya wananchi. Nsekela alisema kuwa kupitia program hiyo Benki ya CRDB imetenga kiasi cha shilingi bilioni 300 kwa miaka mitano, bilioni 60 kila mwaka. Alibainisha kuwa mbali na uwezeshaji huo wa kifedha, programu hiyo pia itahusisha mafunzo ya ujasiriamali ambayo yanaendeshwa katika mikoa yote Zanzibar. “Mheshimwa Rais utaratibu wa mikopo hii ni rahisi sana na tutakuwa tukiitoa kwa kushirikiana na Serikali katika hatua zote za utambuzi na upitishwaji wa mikopo ili kuhakikisha makundi yote stahiki ya wajasiriamali yananufaika,” amesema Nsekela. Akielezea utaratibu wa utoaji mikopo hiyo kupitia programu ya “INUKA”, Nsekela amebainisha kuwa benki hiyo imezingatia mazingira ya soko la Zanzibar na kuwa mikopo itatolewa kupitia mfumo wake wa kutoa huduma unaozingatia misingi ya dini ya kiislamu “CRDB Al Barakah Banking”, pamoja na mfumo wa kawaida kwa wale watakaohitaji. Shughuli zilizopewa kipaumbele katika program hii ya “INUKA” ni zile ambazo zimeanishwa katika sera ya Uchumi wa Buluu ikiwamo; uvuvi, ufugaji wa samaki, pamoja na kilimo cha mwani. Kwa kutambua changamoto zilizozikumba biashara nyingi kutokana na janga la COVID19, Benki pia imeainisha maeneo mengine ya kimkakati ya biashara ambayo yanahitaji kuongezewa nguvu ya uwezeshaji. Kwa kutambua umuhimu wa sekta ya ujasiriamali, Serikali ya Awamu ya 8 ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuwawezesha wajasiriamali Zanzibar kunufaika na fursa zilizopo hususan katika uchumi wa buluu. Baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kuwawezesha wajasiriamali na kuchochea ukuaji wa uchumi Zanzibar ni pamoja na urasimishaji wa wajasiriamali kupitia uanzishwaji wa mfumo wa vitambulisho vya kidijitali kwa wajasiriamali, pamoja na kuanzishwa kwa mfuko wa uwezeshaji wajasiriamali ambapo Serikali imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 50.

Kuhusu Benki ya CRDB Benki ya CRDB ni moja benki zinazoongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki, inatoa huduma kwa wateja wadogo, wakati na wakubwa ikiwamo huduma kwa wateja binafsi, huduma za hazina, huduma za bima, mikopo ya biashara, kilimo na uwezeshaji kwa wajasiriamali wadogo. Benki ya CRDB ndio benki ya kwanza nchini Tanzania kutambuliwa na kampuni ya kimataifa ya utafiti ya Moody’s Investors Service kuwa moja kati ya benki 10 imara na salama Afrika katika uwekezaji. Moody’s imeipa Benki ya CRDB daraja la uimara la B1 ambapo ni daraja la juu zaidi kupatikana kwa mabenki na taasisi za fedha katika ukanda wa jangwa la Sahara. Benki ya CRDB imekuwa kiungo muhimu cha biashara katika nchi za Tanzania na Burundi kwa kuwahudumia wateja zaidi ya milioni 3 na kupitia mtandao mpana wa matawi 268, zaidi ya CRDB Wakala 20,000, 550 ATM, mashine za manunuzi 1,800 na Kituo cha Huduma kwa Wateja kinachotoa huduma saa 24/7.