Benki ya CRDB yawashukuru wateja mafanikio ya huduma bora kwa jamii

By: | Blog | July 23, 2024 10:29

Dar es Salaam Oktoba 3 2022 - Wakati makampuni na taasisi dunia nzima zikiadhimisha ‘Wiki ya Huduma kwa Wateja’ mwaka 2022, Benki ya CRDB imeianza wiki hiyo kwa kuwashukuru wateja wake kwa maoni na ushauri ambao umeiwezesha benki hiyo kutoa huduma bora na zenye viwango vya kimataifa kwa jamii. Salamu hizo za shukrani zimetolewa na Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo wakati wa hafla iliyofanyika katika tawi la Benki hiyo lililopo Oysterbay, Jijini Dar es Salaam. Nshekanabo alisema wateja wamekuwa msingi mkubwa kwa Benki ya CRDB kufikia mafanikio ambayo imekuwa ikiyapata kufikia kuwa ‘Benki Bora zaidi Tanzania’. “Tukiongozwa na kaulimbiu yetu ya ‘Benki inayomsikiliza mteja’ tumekuwa tukipokea maoni na ushauri wa wateja ambao kwa kiasi kikubwa umechangia ubora wa huduma na bidhaa zinazotolewa na benki yetu. Hii inaonyesha ni kwanamna gani mteja amepewa kipaumbele kikubwa katika mkakati wa biashara yetu,” aliongezea Nshekanabo. Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja Benki ya CRDB, Yolanda Uriyo amesema pamoja na kuwashukuru wateja, katika Wiki ya Huduma kwa Wateja mwaka huu wamedhamiria kuwasherekea wale wote walio mstari wa mbele kuiwezesha benki hiyo kutoa huduma bora”. “Wakati dunia nzima ikiadhimisha wiki hii kwa kaulimbiu ya ‘Celebrate Service’ inayomaanisha kusherehekea huduma, kwetu sisi hii ni zaidi ya kaulimbiu kwani mafanikio tuliyonayo yanatulazimisha kuwasherehekea wanaotufanya tuwe bora zaidi; wateja na wafanyakazi wetu,” alifafanua Uriyo. Uriyo alisema Benki ya CRDB itaitumia wiki hii kuwashkuru na kuwasherehekea wateja ambao wamekuwa chachu ya huduma bora zinazotolewa na benki hiyo. Aidha, watakuwa wakiwasherekea wafanyakazi ambao wamekuwa wakitoa huduma bora kwa weledi na ubunifu mkubwa Benki ya CRDB inatajwa kuwa benki inayoongoza kwa huduma bora kwa wateja. Mwaka huu benki hiyo imetunukiwa tuzo ya ‘Benki Bora Tanzania’ na jarida maarufu duniani la nchini Uingereza la Euromoney. Mwaka jana mwishoni benki hiyo ilitunukiwa ‘Tuzo ya Ubora’ na Taasisi ya Utafiti wa Ubora barani Ulaya (European Society for Quality Research). Katika miaka ya hivi karibuni Benki ya CRDB imeweka kipaumbele na kufanya uwekezaji mkubwa katika huduma kwa wateja. Benki hiyo imewekeza katika mifumo ya kisasa na ya kidijitali ya utoaji huduma, ikiwamo mifumo ya mawasiliano, ambayo imesaidia kuongeza ufanisi katika matawi yake zaidi ya 260 yaliyosambaa kote nchini. Uwekezaji huu pia umeongeza ufanisi katika njia mbadala za utoaji huduma; CRDB Wakala zaidi ya 22,000, ATMs zaidi ya 550, na huduma za SimBanking, SimAccount, na Internet banking. “Benki pia imewekeza katika mafunzo kwa wafanyakazi ili kuwawezesha kupata weledi pindi wanapowahudumia wateja. Hii imeenda sambamba na uboreshaji wa taratibu zetu za utoaji huduma (processes) ili ziendane na mahitaji ya wateja,” alisema Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo.

  • MWISHO - Kuhusu Benki ya CRDB Benki ya CRDB ni moja benki zinazoongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki, inatoa huduma kwa wateja wadogo, wakati na wakubwa ikiwamo huduma kwa wateja binafsi, huduma za hazina, huduma za bima, mikopo ya biashara, kilimo na uwezeshaji kwa wajasiriamali wadogo. Benki ya CRDB ndio benki ya kwanza nchini Tanzania kutambuliwa na kampuni ya kimataifa ya utafiti ya Moody’s Investors Service kuwa moja kati ya benki 10 imara na salama Afrika katika uwekezaji. Moody’s imeipa Benki ya CRDB daraja la uimara la B1 ambapo ni daraja la juu zaidi kupatikana kwa mabenki na taasisi za fedha katika ukanda wa jangwa la Sahara. Benki ya CRDB imepata utambuzi wa Mfuko wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UN Green Climate Fund) tangu mwaka 2019 na pia imetambuliwa kama benki bora Tanzania na jarida la Global Finance kwa mwaka 2020. Benki ya CRDB imekuwa kiungo muhimu cha biashara katika nchi za Tanzania na Burundi kwa kuwahudumia wateja zaidi ya milioni 3 na kupitia mtandao mpana wa matawi 268, zaidi ya CRDB Wakala 22,000, 550 ATM, mashine za manunuzi 1,800 na Kituo cha Huduma kwa Wateja kinachotoa huduma saa 24/7.