Baada ya maboresho ya mfumo Benki ya CRDB yawapika mawakala ikizindua huduma ya Tokenization

By: Niels Malangalila | Blog | October 13, 2025 08:01

Baada ya kukamilisha maboresho ya mfumo mkuu wa uendeshaji, Benki ya CRDB imetoa semina elekezi kwa mawakala wake jijini Dar es Salaam sambamba na kuzindua huduma bunifu ya Tokenization inayomruhusu mteja kutuma fedha kwa mtu ambaye si mteja wa Benki ya CRDB ambaye atazitoa kwa wakala wa Benki ya CRDB kwa kutumia namba maalumu ya siri (token) atakayotumiwa baada ya kupokea fedha hizo. Akifungua semina pamoja na kuzindua huduma hiyo, Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Dar es Salaam, Muhumuliza Buberwa amesema mawakala ni jukwaa pendwa la kufikisha huduma kwa wananchi hivyo ni muhimu kuwajengea uwezo wa kuboresha namna wanayowahudumia wateja. Buberwa amesema Benki ya CRDB inao zaidi ya mawakala 45,000 nchini kote ambao kwa mwaka uliopita wamefanikisha zaidi ya miamala milioni 200 yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 72 huku wakitoa huduma sawa na mteja anazozipata akiwa ndani ya tawi la benki. “Benki yetu ya CRDB imeona ni muhimu sana kukutana na mawakala baada ya maboresho ya mfumo mkuu tuliyoyafanya hivi karibuni. Kupitia semina hii, wataalamu wetu watapokea maoni yenu na kujibu maswali mtakayouliza. Biashara hufanyika vizuri zaidi pale mtoa huduma anapopokea maoni ya watu anaowahudumia,” amesema Buberwa. Buberwa amesisitiza kwamba siku zote, Benki ya CRDB itaendelea kuwasikiliza wateja wake na kuboresha huduma ili kukidhi mahitaji na matarajio yao jambo linaloiwezesha kubuni huduma na bidhaa mpya zinazoendelea kutambulishwa kila siku. “Leo tunazindua huduma ya Tokenization inayomruhusu mteja kutoa fedha alizotumiwa kutoka benki nyingine au mtandao wa simu. Huduma hii ni matokeo ya mafanikio ambayo Benki ya CRDB imeyapata baada ya maboresho iliyoyafanya,” amesema meneja huyo wa kanda. Akieleza namna huduma hii mpya inavyomunufaisha mteja, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Uwakala na Malipo wa Benki ya CRDB, Catherine Rutenge amesema kwa muda mrefu mawakala walikuwa wanaweza kuwahudumia wateja wa Benki ya CRDB pekee lakini sasa wigo umetanuliwa. “Mawakala wetu wameenea nchi nzima. Tunafahamu kwamba watu wengi wanamiliki simu za mkononi. Sasa hivi hawa wote wataweza kuhudumiwa iwapo watatumiwa hela na mteja wetu. Kutokana na idadi kubwa ya wateja tuliyonayo tunaamini huduma hii itawagusa watu wengi zaidi hata wale wasio wateja wa Benki yetu ya CRDB,” amesema Catherine. Tokenization ni mwendelezo wa uwezeshaji wa wateja wa Benki ya CRDB kutuma miamala kwa watu ambao si wateja wa benki. Kwa sasa, wateja waliotumiwa hela kwenye simu zao wanaweza kuzitoa kwenye mashine ya kutolea fedha au ndani ya benki kwa kutumia namba ya siri waliyotumiwa. Katika mwendelezo huu, Catherine amesema fedha atakayotumiwa mteja haitahusika kwenye makato ya madeni aliyonayo kwani haiingii na kujumuishwa na salio alilonalo bali inaingia ili azitoe kwa wakala ndani ya saa 48 yaani siku mbili. “Ni kawaida mtu kusema usinitumie kwenye namba hii kwani inadaiwa. Tunalifahamu hilo ndio maana tumelizingatia. Kwenye huduma yetu ya Tokenization, mpokeaji atatoa hela yake yote kama alivyotumiwa. Nitumie fursa hii kuwakaribisha wale ambao si wateja wetu wajiunge na Benki ya CRDB ili kufurahi ubunifu huu tunaoendelea kuuleta sokoni kila siku,” amesisitiza Catherine. Akizungumza kwenye semina hiyo, Flora Erasto ambaye ni wakala mkuu wa Benki ya CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya GAF amesema maboresho yanayoendelea kufanywa yanawawezesha kuhuisha akaunti ya mteja, kumsajili mteja kwenye Simbanking, kufungua akaunti na kupata huduma nyingi nyingine. “Semina hizi zinazotolewa zinatusaidia sana kukabiliana na changamoto zinazojitokeza pindi tunapowahudumia wateja wetu. Hata mfanyakazi akiondoka au kukiwa na dharura yoyote, mmiliki anaweza kutoa huduma kama kawaida. Inakuwa changamoto kwa mawakala ambao hawahudhurii mafunzo kwani hukwama kwenye maeneo ambayo wenzao wanaweza kutatua chochote kinachosumbua. Nawahimiza mawakala wenzangu kujitokeza kila zinapofanyika semina hizi,” amesema Flora. Baada ya uzinduzi wa semina hiyo jijini Dar es Salaam, Benki ya CRDB itaendelea kuwafikia mawakala wake katika kanda zote ili kuwajengea uwezo wa kuboresha huduma mawakala wake wanaohudumia zaidi ya wateja milioni 6 kote nchini. Semina hizi zitaendelea kufanyika mpaka Desemba na kuwaruhusu mawakala kutengenezewa mashine zao zilizoharibika au kupata changamoto nyingine bila malipo yoyote.

What's new?

...
BLOG
Wateja wapongeza Mageuzi ya Mfumo Benki ya CRDB ikisherehekea Wiki ya Huduma kwa Wateja

...

Read More
...
BLOG
CRDB Bank Formalizes Strategic Partnership with Japan's Sumitomo Mitsui Banking Corporation

Yokohama, Japan – August 21, 2025 – We at CRDB Bank PLC are excited to announce a historic milestone...

Read More
...
BLOG
Fahad Soud Hilal wa Tanga Anyakua Toyota IST Kupitia Kampeni ya Benki ni Simbanking ya CRDB

...

Read More