Benki ya CRDB yazindua programu ya uwezeshaji kwa vijana na wanawake wajasiriamali kiuchumi iliyopewa jina la "Imbeju"
By: | Blog | January 22, 2025 11:42
Zanzibar 28 Oktoba 2022 – Ikiendeleza jitihada zake za kukuza ujumuishi wa kiuchumi nchini, Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Tume ya TEHAMA imezindua programu mpya ya uwezeshaji kwa vijana na wanawake wajasiriamali, Sh. bilioni 5 zatengwa. Programu hiyo iliyopewa jina la ‘IMBEJU’ imezinduliwa katika kilele cha Kongamano la Sita la TEHAMA lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Golden Tulip na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na taasisi kutoka ndani na nje ya nchi. Akielezea kuhusu programu hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kupitia ‘IMBEJU’, benki hiyo itakuwa ikitoa mitaji wezeshi kwa vijana na wawawake wajasiriamali wenye biashara na mawazo bunifu. Nsekela alisema kupitia programu hiyo vijana watakuwa wakiwasilisha mpango wa biashara zao, na mawazo bunifu kwa upande wa wanafunzi, kisha wataalamu wabobezi watakuwa wakichambua na kuidhinisha mtaji na mafunzo kulingana na vigezo. “Katika programu ya IMBEJU tutakuwa pia tukitoa mafunzo ya usimamizi wa biashara, matumizi ya mifumo ya TEHAMA, elimu ya fedha na masoko, na usaidizi wa kuboresha bidhaa na mawazo bunifu,” alisema Nsekela. Aliongezea kuwa Benki hiyo pia imeanzisha kituo maalum cha mafunzo na ubunifu wa biashara katika Makao Makuu ya zamani ya Benki hiyo mtaa wa Azikiwe jijini Dar es Salaam. Kituo hicho kitasimamiwa kwa ushirikiano na Tume ya TEHAMA nchini. “Katika programu za vijana wajasiriamali tumeweka mkazo mkubwa zaidi katika biashara zinazoanza katika sekta ya TEHAMA tukilenga zaidi kuchochea uchumi wa kidijitali. Biashara katika sekta nyengine pia zitakuwa zikipata uwezeshaji,” alifafanua. Kwa upande wa uwezeshaji wa wanawake wajasiriamali, Nsekela alisema Benki hiyo itakuwa ikifanya kazi na taasisi na mashirika yaliyojikita katika kufanya uwezeshaji kwa wanawake. Uwezeshaji utafanyika kwa vikundi na wajasiriamali mmoja mmoja. Kwa kuanzia katika uzinduzi huo wa programu ya IMBEJU Benki ya CRDB imekabidhi jumla ya shilingi milioni 50 kwa Tume ya TEHAMA ikiwa ni uwezeshaji kwa biashara change katika sekta ya TEHAMA (digital startups). Akizindua programu hiyo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuanzisha programu hiyo ya ‘IMBEJU’ akisema itasaidia kukuza ujumuishi wa kiuchumi kwa vijana na wanawake. “Idadi kubwa ya watu hapa nchini ni vijana na wanawake. Licha ya hivyo ndio watu tegemezi zaidi kiuchumi. Serikali imekuwa ikiweka jitihada kubwa katika kuliwezesha kundi hili. Niipongeze Benki ya CRDB kwa kuunga mkono,” alisema. Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga alisema wamejipanga vilivyo kuhakikisha programu ya ‘IMBEJU’ inakwenda kuchochea kwa kasi ukuaji wa biashara changa nchini. IMBEJU inaenda sambamba na kauli mbiu ya “Leave No One Behind” ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SGD) 2030 inayosisitiza uwezeshaji kwa makundi yaliyotengwa na kukabiliana na ukosefu wa usawa katika fursa za kiuchumi. -MWISHO- Kuhusu Benki ya CRDB Benki ya CRDB ni moja benki zinazoongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki, inatoa huduma kwa wateja wadogo, wakati na wakubwa ikiwamo huduma kwa wateja binafsi, huduma za hazina, huduma za bima, mikopo ya biashara, kilimo na uwezeshaji kwa wajasiriamali wadogo. Benki ya CRDB ndio benki ya kwanza nchini Tanzania kutambuliwa na kampuni ya kimataifa ya utafiti ya Moody’s Investors Service kuwa moja kati ya benki 10 imara na salama Afrika katika uwekezaji. Moody’s imeipa Benki ya CRDB daraja la uimara la B1 ambapo ni daraja la juu zaidi kupatikana kwa mabenki na taasisi za fedha katika ukanda wa jangwa la Sahara. Benki ya CRDB imepata utambuzi wa Mfuko wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UN Green Climate Fund) tangu mwaka 2019 na pia imetambuliwa kama benki bora Tanzania na jarida la Global Finance kwa mwaka 2020. Benki ya CRDB imekuwa kiungo muhimu cha biashara katika nchi za Tanzania na Burundi kwa kuwahudumia wateja zaidi ya milioni 3 na kupitia mtandao mpana wa matawi 268, zaidi ya CRDB Wakala 22,000, 550 ATM, mashine za manunuzi 1,800 na Kituo cha Huduma kwa Wateja kinachotoa huduma saa 24/7.