Wanahisa Benki ya CRDB kukutana Arusha, kushiriki mtandaoni Mkutano Mkuu wa 31
By: Niels Malangalila | Blog | May 14, 2026 09:36
Ikiwa na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi, Benki ya CRDB inatarajia kufanya Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa siku ya Jumamosi, tarehe 16 Mei 2026 kuanzia saa 2 asubuhi katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC). Taarifa hiyo imetolewa leo katika mkutano na waandishi wa habari uuliofanyika hoteli ya Mount Meru ambapo Benki ya CRDB pia ilizindua Ripoti yake ya Mwaka na Ripoti ya Uendelevu kwa mwaka 2025.
Mkutano huo unafanyika kufuatana na Sheria ya Makampuni namba 212 ya mwaka 2002, ambapo kila mwaka Benki ya CRDB imekuwa ikiandaa mkutano huo unaowapa Wanahisa fursa ya kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupitisha au kuidhinisha maamuzi mbalimbali yenye maslahi kwa Benki. Akizungumzia katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika hoteli ya Mount Meru jijini Arusha, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori amesema utafanyika kwa njia mseto (Hybrid Meeting) ili kutoa fursa kwa wanahisa watakaoshindwa kufika ukumbini kushiriki kwa njia ya mtandao. Prof. Mori alisema kupitia mtandaoni Wanahisa wataweza kujiunga kuanzia saa 2:00 asubuhi kupitia link https://escrowagm.com/crdb/login.aspx au kupitia SimBanking App, ambapo imewekwa sehemu ya ya kujisajili kushiriki Mkutano Mkuu. “Tumeweka mwongozo wa jinsi ya kushiriki mkutano mkuu kwa njia ya mtandao kupitia tovuti yetu ya www.crdbbank.co.tz, mitandao yetu ya kijamii, na maelekezo yametumwa kwa ujumbe mfupi kwa wanahisa wote,” alisema Prof. Mori huku akiwahakikishia wanahisa kuwa watashiriki bila chanagamoto yoyote. Ajenda mbalimbali zitajadiliwa katika Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB ni pamoja na uchaguzi wa mjumbe huru wa bodi, kuteua wakaguzi wa hesabu, na kujadili na kupokea Taarifa ya Bodi ya Wakurugenzi, na Taarifa ya Hesabu zilizokaguliwa, pamoja na gawio kwa mwaka 2025 ambapo pendekezo la gawio la Shilingi 90 kwa kila hisa moja litawasilishwa sawa na ongezeko la asilimia 38 kulinganisha na Sh 65 mwaka 2024. Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, alisema pendekeo hilo la ongezeko la gawio kwa hisa linatokana na Benki ya CRDB kuendelea kupata matokeo mazuri sokoni ambapo mwaka wa fedha ulioisha ilipata faida baada ya kodi ya Shilingi 728.6 bilioni ukilinganisha na Shilingi 551 bilioni mwaka 2024. Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB utatanguliwa na Siku maalum ya Uwekezaji kwa Wanahisa wa Benki ya CRDB kwa wanahisa na umma yenye kaulimbiu ya “Vijana na Uwekezaji katika Hisa” itakayofanyika siku ya Ijumaa tarehe 15 Mei 2026 kuanzia saa 2 asubuhi katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC). Prof. Mori amesema Siku hiyo ya Uwekezaji itafunguliwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Mussa Nsekela, amewahimiza wanahisa kushiriki kikamilifu Mkutano Mkuu huo pamoja na Siku ya Uwekezaji kwa Wanahisa, huku akitoa wito kwa vijana kujitokeza katika jukwaa hilo muhimu. Amesema Siku ya Uwekezaji ya mwaka huu imeandaliwa mahsusi kwa ajili ya vijana ili kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa uwekezaji katika hisa, masoko ya mitaji pamoja na nafasi yao katika kujenga uchumi wa Taifa kupitia uwekezaji wa muda mrefu. Dkt. Nsekela alisema Benki ya CRDB inaamini kuwa vijana wanapaswa kuwa sehemu ya kizazi cha wawekezaji kitakachoendeleza mafanikio ya taasisi za Kitanzania katika miaka ijayo, ndiyo maana Benki imeendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuwaelimisha na kuwajumuisha vijana katika uwekezaji, ujasiriamali na uchumi rasmi wa nchi.
What's new?
BLOG
CRDB Bank launches “Benki Kimpango Wako”, pledging enhanced services for customers and stakeholders in 2026
...
Read More